Thursday, 5 December 2013

"Propaganda zinazoendelea sasa hivi zinatuimarisha CHADEMA"......Dk. Slaa

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kamwe chama hicho hakitakubali kuwa legelege katika kusimamia misingi yake, ikiwemo katiba inayowaunganisha wanachama wote.

Alisema kuwa licha ya kuzushiwa propaganda nyingi ikiwemo udini na ukabila, lakini chama hicho kimefanikiwa kuzishinda hali aliyoelezea imewakomaza katika safari yao ya kuchukua madaraka.


Kauli hizo alizitoa jana mjini Kahama mkoani Shinyanga alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya CDT, ikiwa mwanzo wa ziara yake ya kukiimarisha chama.

Dk. Slaa alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010, chama hicho kiliwaahidi Watanzania kuwa kama kingeshika dola, kingekuwa imara kusimamia serikali itakayowatumikia wananchi.

Alibainisha kuwa ili kuitimiza ahadi hiyo, chama hicho kamwe hakiwezi kuwa legelege kwa wanachama na viongozi wasiotaka kufuata katiba na taratibu za chama.

“Watanzania tulieni, tulieni, tulieni. Chama hiki kipo kwa ajili ya kuwatumikia ninyi na kusimamia maslahi yenu. Acheni ushabiki kwenye masuala mazito,” alisema.
Dk. Slaa alisema amekuwa akipigiwa simu na watu wengi wakimuulizia hali ya mambo inavyokwenda ndani ya chama hicho, hasa baada ya uamuzi wa Kamati Kuu kuwavua uongozi baadhi ya makada wake akiwemo mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

“Mimi nawaambia watulie tu… Nawaambia waviamini vikao vya chama chao, ndani ya CHADEMA hakuna mtu mkubwa kuliko katiba. Wote hapa tunaunganishwa na katiba.

“Chama hiki kimepita kila aina ya propaganda ikiwemo hii ya juzi ya ugaidi, zote tumezishinda na tutaendelea kuzishinda. Hata hii ya sasa inayosukumwa na mipango ya hujuma inayopangwa na CCM, wakishirikiana na vyombo vya dola na watendaji wa serikali, tunazidi kuimarika na kutukomaza kwenda kushika dola.

“Wakati wa kampeni mwaka 2010 tuliwaambia Watanzania kuwa tunakwenda kusimamia maslahi ya Watanzania. Tulisema elimu bure, mwaka jana wameamua kutuiga, tulisema vifaa vya ujenzi vishuke, pia wameamua kutuiga, lakini wameshindwa kutekeleza,” alisema.

Dk. Slaa alisema kuwa CCM wameshindwa kutekeleza kile kilichokuwa kikisemwa na CHADEMA, ambayo sasa inaamini ikiingia madarakani itatimiza mambo iliyowaahidi wananchi.
Safari yapata matatizo.

Ziara ya Dk. Slaa jana iliingia dosari baada ya magari aliyokuwa akiyatumia kupata hitilafu za kiufundi zilizosababishwa na kile kinachodaiwa ni mafuta machafu waliyoyaweka katika kituo kimoja cha mafuta kilichopo wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Mafuta hayo yaliyafanya magari yaliyokuwa kwenye msafara huo kushindwa kwenda mwendo uliotarajiwa, na hivyo kusababisha Dk. Slaa na timu yake kufika katika viwanja vya mkutano saa 12 jioni.

Dk. Slaa leo anatarajia kwenda mkoani Kigoma ambako atahutubia mikutano mbalimbali ya hadhara pamoja na kufanya shughuli za kuimarisha chama kila eneo atakalolitembelea.

0 comments:

Post a Comment