Friday 29 November 2013

UTAFITI: HAYA NDIO MADHARA YA INTERNET KWA VIJANA...SOMA HAPA KUYAFAHAMU...

 

MAMILIONI ya vijana duniani kote wanatumia intaneti, iwe nyumbani, shuleni, kwenye nyumba za marafiki au kwenye simu zao za mikononi.
Huenda watoto wako wanaielewa sana dunia ya intaneti kuliko wewe, na hata wanaweza kukuficha mambo wanayoyafanya kwenye intaneti.


Hata hivyo unaweza kujua mambo yanayowahangaisha vijana na watoto kwenye intaneti na si lazima uwe mtaalamu wa vifaa vya elektroniki ili uweze kumlinda mtoto wako.
Katika nchi zilizoendelea wakati fulani ilionekana kwamba ingekuwa salama kutumia intaneti ikiwa kompyuta ingekuwa mahali palipo wazi. Ilifikiriwa kwamba ukifanya hivyo haitakuwa rahisi kwa watoto na vijana kufungua vituo visivyofaa.

Bado wazo hilo linafaa kwa kuwa si jambo linalopatana na akili kuwaruhusu watoto kutumia intaneti katika chumba chao cha kulala. 

Jambo unaloweza kufanya 
Ukiwa mzazi au mlezi kuna mambo mawili ya hatari kuhusu intaneti ambayo yanahitaji mtu awe mwangalifu.
Wazazi hawawezi siku zote kuwazuia watoto wao kuendesha gari, lakini wanaweza kuhakikisha kwamba watoto wao wamefundishwa kuendesha gari kwa njia salama. Wazazi wengi wamechukua hatua kama hiyo kuhusu matumizi ya intaneti.

Michel ni mama anayeishi California, Marekani, ni mhasibu katika shule moja kubwa jimboni humo.
Anasema: “Kwa kawaida nimewatengea muda watoto wa kuangalia intaneti na ninaongea nao mara kwa mara kuhusu vituo visivyofaa na watu wanaoweza kukutana nao katika vituo mbalimbali wasio na nia nzuri kwao na pia madhara ya intaneti.”

Michel anasema ni jukumu la kila mzazi au mlezi kuhakikisha watoto wao hawafungui vituo visivyofaa na kuhakikisha wanawapa malezi mema na yenye maadili.
Wazazi ambao watoto wao wanatumia intaneti wanahitaji kujua mambo ya msingi kuhusu intaneti na watoto wao wanafanya nini wanapotuma ujumbe mfupi wanapofungua tovuti katika intaneti.

“Usikate kauli kwamba wewe ni mzee sana au huna elimu ya kutosha kujifunza,” anasema Marshay, mama mwenye watoto wawili, na kuongeza kuwa hutakiwi kuachwa nyuma na teknolojia.

“Watu wanaotoa huduma za intaneti na programu za kompyuta wametengeneza programu zinazoweza kuchuja au kuzuia ujumbe unaokuambia ufungue tovuti zisizofaa.
“Programu fulani zinaweza hata kumzuia mtoto asitoe habari za kibinafsi kama vile jina au anuani yake. Hata hivyo , mzazi anapaswa kujua kuwa vichujio hivyo havichuji habari zote mbaya. Pia, watoto wengine walio na ujuzi wa kompyuta wanaweza kujua jinsi ya kuepuka programu hizo,” anasema.

Huko Uingereza, asilimia 57 ya vijana walio na umri wa kati ya miaka 9 na 19 wanaotumia intaneti kila juma wamepata ponografia (picha za ngono), hata hivyo ni asilimia 16 tu ya wazazi wanaoamini kwamba mtoto wao ameona ponografia kwenye intaneti.

Wazazi wanapaswa kukumbuka kwamba vijana wengi wanaweza kutumia intaneti kupitia simu zao za mikononi. Simu za mikononi na intaneti licha ya kurahisisha wawasiliano pia zimekuwa ni kero, shuleni, kazini, nyumbani na sehemu nyingine muhimu.

Katika familia mbalimbali kazi za nyumbani zimekuwa zikifanyika kiuzembe na kuchelewesha muda wa chakula, hasa mwenye nyumba anapokuwa hayupo.

Nilipokuwa Morogoro mbali kabisa na mji, nilishuhudia katika familia moja msaidizi wa kazi za nyumbani jinsi anavyotumia muda mwingi kwa kusoma na kujibu ujumbe mfupi anaotumiwa.

Binti anayetarajia kujiunga na chuo kimojawapo hapa nchini anatumia muda mwingi kuwasiliana na marafiki, nilipompa kitabu cha kujisomea jibu lake lilinishtua alisema hivi: “Nimejaribu kusoma lakini sijaelewa chochote.” Akanirudishia kitabu.

Hao ni mfano mdogo sana kwa watoto wetu. Licha ya kuudhi wanafunzi katika vyuo mbalimbali hapa Tanzania wanapoteza muda wao mwingi sana kwa matumizi ya simu za mkononi na intaneti.
Uchunguzi uliofanywa Uingereza ulionesha kwamba kijana mmoja kati ya watano anaweza kutumia intaneti katika chumba chake cha kulala.

Lakini inaelezwa kwamba kuweka kompyuta mahali palipo wazi kunawasaidia wazazi kuchunguza kile ambacho watoto wao wanafanya kwenye intaneti na kuweza kuwatia moyo na kwafundisha wajiepushe na vituo visivyofaa.

Weka wakati ambao watoto wanaweza kutumia intaneti muda wanaopaswa kuitumia na vituo ambavyo hawapaswi kuvifungua.
Zungumzia sheria zako hizo pamoja na watoto wako, na uhakikishe kwamba wamezielewa na kuzifuata kwa manufaa yao na kwa wengine.

Bila shaka huwezi kuwachunguza watoto wako wasipokuwa nyumbani. Hivyo ni muhimu kuwafundisha kanuni zinazofaa ili wafanye maamuzi yenye heshima na hekima wakati ambao wewe uko mbali nao.

Wazazi wawaeleze watoto wao matokeo ya kuvunja sheria kuhusiana na intaneti na mambo mengine muhimu yatakayowasaidia maishani mwao.
Pia mzazi unapaswa kuchunguza jinsi watoto wake wanavyotumia intaneti na uwaeleze kwamba utakuwa unawachunguza. Kufanya hivyo si kuingilia faragha yao.
Kumbuka kwamba intaneti hutumiwa na watu wote. Shirika la Upelelezi la Marekani linapendekeza kwamba wazazi wanapaswa kuchunguza akaunti za watoto wao za intaneti, barua pepe zao na tovuti ambazo wanafungua.

Raymond Rugemalira Mwijage ni mwanasayansi na profesa anayeishi California, Marekani anasema: “Nyumbani kwangu nimetenga muda maalumu wa familia yangu kuangalia runinga na kufuatilia kwa ukaribu kila mwanafamilia anachofanya kwenye intaneti.”

Anasema huwezi kuchunguza jinsi mtoto wako anavyotumia intaneti kila wakati. Hivyo, ni viwango unavyofundisha na mifano unayotoa ndivyo vitawalinda watoto wako zaidi.
Mwijage anasema tenga wakati wa kuzungumza na watoto wako kuhusu hatari za intaneti.

Njia bora zaidi za kuwalinda watoto wako dhidi ya hatari za intaneti ni kuwasiliana nao waziwazi.
Anasema: “Tulizungumza na wavulana wetu kuhusu watu wabaya kwenye intaneti. Pia tuliwaeleza ponografi ni nini, kwa nini wanapaswa kuiepuka na kwa nini hawapaswi kamwe kuwasiliana na watu wasiowajua.
“Intaneti imekuwa pia ikipotezea watu muda wa kufanya kazi. Nilipokuwa namuuguza ndugu yangu katika hospitali moja kubwa (jina limehifadhiwa) jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, jopo la madaktari limemzunguka mgonjwa, cha kushangaza mmoja wao hana muda na kinachoendelea, yuko ‘busy’ na simu yake ya mkononi akichati.”

Madhara ya simu za mkononi yameathiri sana sekta ya elimu kwa nchi nyingi duniani.
Inasikitisha sana nchi zinazoendelea zimekuwa wahanga wakubwa wa janga hili; nilipokuwa mkoani Morogoro (vijijini ) Tanzania kwa tafiti, ikiwamo elimu, nilichokabiliana nacho cha kutisha ni simu za mkononi, runinga na tamthilia ni moja ya mambo makuu yanayosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu.

Unaweza kuwalinda watoto
Jitihada zinahitajika ili kuwalinda watoto wako kutokana na hatari za intaneti na njia ya kupata habari kupitia vifaa vya elektroniki inabadilika kila mara.
Huenda pia teknolojia mpya ikawa na faida na hatari nyingi sana kwa watoto.

Wazazi wanaweza kuwaandaa watoto wao kwa ajili ya hatari watakazokabiliana nazo wakati ujao.
Hekima ni ulinzi kama vile pesa ni ulinzi pia. Wasaidie watoto wako kuwa na hekima ili waweze kupambanua zuri na baya.

Pia wasaidie waelewe jinsi ya kuepukana na hatari za intaneti na jinsi ya kuitumia kwa njia inayofaa.
Kwa namna hii, intaneti inaweza kuwa kifaa kizuri ambacho hakitahatarisha usalama wa watoto wako.
Wataalamu wanaamini kwamba huenda kila siku zaidi ya watu 750,000 wanaovizia watoto ili wawarubuni kufanya nao ngono wanatumia vituo vya maongezi na vituo vya kuwatafutia watu wachumba.

Marekani, zaidi ya asilimia 93 ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17 wanatumia intaneti.
Katika nchi zinazoendelea, intaneti imegeuka pia kuwa kero na kuathiri maendeleo mazuri kimasomo na maisha ya vijana, watoto na watu wazima kwa ujumla.


0 comments:

Post a Comment