Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amejiweka katika mazingira magumu zaidi kisiasa ndani ya chama hicho, kutokana na shaka kubwa iliyougubika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam juzi.
Zitto
pamoja na viongozi wengine wawili wa Chadema; Dk Kitila Mkumbo na
Samson Mwigamba walivuliwa nyadhifa zao na Kamati Kuu ya Chadema baada
ya kubainika kupanga mbinu za uasi, kupitia waraka ambao ulikuwa
ukieleza mkakati wa kufanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi wakati wa
uchaguzi mkuu wa ndani.
Leo,
uongozi wa Chadema umeitisha mkutano wa waandishi wa habari ambao
pamoja na mambo mengine, utajibu baadhi ya hoja za utetezi ambazo
zilitolewa na Zitto pamoja na Dk Kitila. Katika mkutano wa juzi, Zitto
na Dk Kitila ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,
walizungumzia kuvuliwa kwao madaraka, lakini maandalizi na uendeshaji wa
mkutano huo yanazua shaka kutokana kuwahusisha watu wanaodaiwa kuwa ni
wanachama wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Miongoni
mwao, wamo waliowahi kuwa wanachama wa Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha), Habib Mchange na Mtela Mwampamba ambao walitimuliwa kwa
makosa yanayofanana na yale yalizosababisha Zitto na wenzake kuvuliwa
nyadhifa zao.
Mchange
na Mwampamba pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana
Shonza, walivuliwa uanachama wa Baraza hilo Januari 5, mwaka huu baada
ya kupatikana na hatia ya kutumia mitandao ya kijamii kukihujumu Chadema
na kuwatukana viongozi wake wakuu. Baadaye walihamia CCM wanakoendeleza
harakati zao za kisiasa.
Jana,
Machange alipotafutwa, alisema: “Mimi sikuwahi kuondoka Chadema,
nilifukuzwa kihuni kama walivyowafanyia Zitto na Kitila. Nimepeleka
malalamiko yangu tangu Januari hadi leo sijajibiwa, hivyo siwezi kusema
nimeondoka.
Nataka nimuunge mkono mwathirika mwenzangu kama ilivyokuwa mimi lakini nitabakia kuwa mwanachama mwaminifu.
“Mimi
ni mwanaChadema na sikuwahi kujiunga na CCM au chama chochote,
walioondoka ni Mwampamba na Shonza.” Mwampamba alisema: “Nilijitokeza
pale kuonyesha mshikamano kwa sababu mimi pia ni mwathirika. Kwa hiyo
nilitaka ulimwengu ufahamu kuwa mimi ni kati ya wanaopinga siasa za aina
hii... Chadema ni chama kinachojiandaa kuchukua dola, sasa kama kila
mwenye mawazo tofauti anaonekana mhaini itakuwaje siku wakichukua dola?
Ubaguzi huu haujalishi uko chama gani, hata kama niko CCM, hilo
halinizuii kuungana na mtu aliyepatwa na tatizo kama langu.”
Kuwepo
kwao katika mkutano wa Zitto kunaweza kutumiwa na uongozi wa Chadema
kuwa uthibitisho wa kiongozi huyo kushiriki katika uasi na kunaweza
kupuunguzia nguvu utetezi unaotolewa na Dk Kitila kwamba hakuwa sehemu
mpango wa kuuondoa uongozi wa sasa madarakani. Zitto, Dk Mkumbo na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba
wanasubiri kukabidhiwa barua za kuvuliwa kwao madaraka na katika siku 14
wanapaswa wawe wamewasilisha utetezi wao wakieleza kwa nini wasifukuzwe
uanachama kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Dk Slaa
Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alisema jana kuwa ilikuwa lazima
viongozi hao wavuliwe madaraka hasa baada ya Dk Kitila kukiri kuhusika
na waraka ambao anasema ulilenga kushinda kupitia uchaguzi halali ndani
ya chama hicho.
“Hata
katika ya nchi ukihusika kutengeneza mbinu za siri lazima
ushughulikiwe.Hakuna Katiba itakayokuruhusu kufanya mipango ya siri.
Kwanza uchaguzi wa Chadema nani katangaza mpaka mipango ianzwe
kutengenezwa sasa hivi?” alihoji Dk Slaa.
-----Mwananchi
-----Mwananchi
0 comments:
Post a Comment