MWALIMU wa shule ya msingi Nyarero katika tarafa ya Inchage wilayani Tarime mkoani Mara, Joshua Makuri (34), amekutwa amekufa na mwili wake kutelekezwa katika maeneo ya uwanja wa shule ya msingi Turwa Tarime.
Katibu tarafa ya Inchage, Jonathan Machango, alisema jana kuwa mwili wa marehemu uligundulika mwishoni mwa wiki iliyopita na watu waliokuwa wakipita karibu na maeneo ya viwanja vya shule ya msingi Turwa.
Mwili huo kwa mujibu wa Machango, ulikutwa na majeraha ambapo jicho moja lilikuwa limetobolewa.
Machango alisema watu hao walipoona mwili huo, walitoa taarifa Polisi ambapo askari walifika na kuuchukua na baada ya muda ndugu za marehemu walijitokeza kuutambua katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya Tarime.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa maalumu wa Tarime Rorya ACP, Sweetbelt Njewike, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuongeza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini waliohusika na tukio hilo.
Mwalimu Makuri alikuwa akifundisha katika Shule ya Msingi Nyarero na mwili wake ulichukuliwa na ndugu zake kwa maziko yaliyotarajiwa kufanyika katika kijijini cha Nyarero.
---HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment