Thursday, 13 March 2014

UTAGUNDUAJE KAMA UNA MIMBA CHANGA?

Mara nyingi ni vigumu mwanamke kugundua kama ameshika mimba siku za mwanzoni hadi pale anapokosa kuona siku zake za hedhi. pamoja na ugumu huo kuna dalili ambazo zinaweza kufanya uhisi kama una mimba katika siku za mwanzoni ambazo ni kuanzia  siku ya 18 toka mimba itungwe.

Dalili hizi zinatofautiana kwa kila mtu, wapo ambao wanaweza kuzipata zote na ambao hupata baadhi tu ya dalili hizi na pia wapo ambao hawazipati kabisa.

Miongoni mwa dalili hizo ni pamoja na:

1.JOTO LA MWILI KUPANDA.(basal body temperature stay high)

   Wanawake wengi hushindwa kutambua dalili hii pale wanapoipata kutokana na kutokuwa na uelewa
    juu ya miili yao.
    Hali hii inaonekana katika siku za mwanzo ambambo huweza kudumu kwa muda mrefu kiasi hivyo
    kama itadumu zaidi ya siku 18 basi ni vizuri kupima ili kujua kama inatokana na ujauzito au la.

2. KUPATA HAJA NDOGO MARA KWA MARA.(frequent urination)
    Kubanwa na haja ndogo mara kwa mara pia inaweza ikawa ni dalili mojawapo ya kuwa na mimba
    changa.

3.KUWA MWEPESI KUHISI HARAFU YA VITU  MBALI MBALI HASA  HARUFU MBAYA.(sensitivity to odors)
   Wakati wa mimba changa wanawake wengi wanakuwa wepesi wa kuhisi harufu ya vitu mbali mbali hasa zile harufu zisizo za kupendeza na kumfanya achukie vitu vingi vyenye kutoa harufu hizo.
 wakati kama huu si ajabu ukaona mtu hataki mume wake amsogelee kwa kudai anatoa harufu mbaya.
ukiona dalili kama hii inaweza ikawa ni ishara ya kuwa mjamzito hivyo unapaswa kufanya uchunguzi.

4.KUKOSA HEDHI.(missed period)
  Kwa kawaida mama mjamzito hapati siku zake za hedhi isipokua anaweza akapatwa na hali ya kuvuja kunakofanana na ile ya hedhi ila damu yake huwa nyepesi sana na hudumu kwa muda mfupi kati ya siku1 au 2 (implantation bleeding) hivyo    unapokosa kuona siku zako za hedhi
  unapaswa kuchunguza sababu za kukosekana kwa hedhi.

5. KICHEFU CHEFU AU KUTAPIKA.( Nausea or vomiting)

Thursday, 27 February 2014

HUMAN PAPILOMA VIRUS INFECTION.

Ugonjwa huu husababishwa na kirusi aitwaye HPV(Human Papiloma Virus), kuna aina 90 za kirusi huyu lakini aina 4 ndio huonekana mara kwa mara(HPV-6, HPV-11, HPV-16 na HPV-18)
Mara nyingi husababisha viotezo mfano kwenye picha inaweza kua kimoja au vingi mfano hapo kwenye picha, hutokea sehemu za haja ndogo, kubwa na sehemu za uzazi(uke, uume, mfuko wa uzazi)
Dalili huonekana kuanzia miezi 3 mpaka miaka 2 baada ya maambukizi

Kuzaa


Vifo vya akina mama wakiwa na Mimba Vinapungua!
Utafiti wa mwaka 2010 wa Hali ya Afya ya Jamii  (UHAJ)  waonyesha mafanikio huduma za Uzazi
Utafiti wa Hali ya Afya ya Jamii 2010 (UHAJ) au kwa Kizungu DHS unaonyesha mafanikio makubwa hasa katika nyanja nne: mahudhurio  ya kliniki wakati wa kujifungua, kujifungulia hospitali, kujifungua ukisaidiwa na mhudumu wa afya yaani nesi au daktari na kupunguza vifo vya akina mama wenye mimba na wakati wa kujifungua
Kuhudhuria kliniki ya uzazi  na kupima mimba ni huduma muhimu ambapo wafanyakazi wa afya, manesi na madaktari wanampima mama na kumfuatilia ili kuyazuia matatizo yanayojitokeza wakati wa mimba, kuyatambua na kuyatibu mapema.  Kwa kupima na kufuatilia mimba kutoka inapotungwa mpaka mtoto anapozaliwa kunazuia na kupunguza matatizo yanayoweza kutokea kwa mama na mtoto wakati wa mimba, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Hapa kwetu Tanzania karibu akina mama wote wenye mimba, kiwango cha tisini na sita kwa mia (96%) hupimwa mimba yaani huhudhuria kliniki ya kina mama wenye mimba angalau mara moja wakati wakiwa na mimba. Utafiti wa Hali ya Afya  ya Jamii (UHAJ) wa   2004-05;  kiwango hiki kilikuwa tisini na nne kwa mia (94%) kwa hiyo UHAJ wa mwaka 2010  umeonyesha ongezeko kidogo  la  mbili kwa mia (2%). Ni vizuri kuona kuwa kuhudhuria kliniki wakati wa mimba ni moja ya huduma ambazo akina mama wana mwamko sana nazo wawe wa kijijini au wa mjini; wenye uwezo kiuchumi au wasio na uwezo wa kiuchumi,  wenye uwezo sana au wenye uwezo hafifu; wote huhudhuria kliniki wakati wakiwa na mimba
Mimba ya miezi saba
Usafi wakati wa kujifungua
Kujifungua kwenye hali ya usafi na pahala ambapo kuna huduma ya daktari au nesi kunapunguza sana uwezekano wa kupata matatizo wakati wa kujifungua yaani matatizo kwa mama na kwa mtoto. Inapunguza sana uwezekano wa kudhurika mama au mtoto. Mama akijifungulia nyumbani, akijifungulia mahali ambapo siyo pasafi; panapokosekana vifaa muhimu na wataalamu yaani daktari au nesi; mama na mtoto wana uwezekano wa kupata madhara ya kuumia na kupata maambukizi ya bakteria, virusi au fangasi.
Nusu ya mama wanaojifungua Tanzania yaani hamsini kwa mia (50%) huzalia kwenye kituo cha huduma za afya yaani hospitali, kituo cha afya au zahanati. Nusu yaani 50% huzalia  nyumbani. Hii tena ni ongezeko kutoka  UHAJ wa  2004-05 ulioonyesha kuwa arobaini na sita kwa mia (46%) ya akina mama wenye mimba  walikuwa wanazalia hospitali na 54% walikuwa wanazalia nyumbani.
Huyu mtoto amezaliwa sasa hivi
Kuna tofauti kati ya akina mama wanaozalia nyumbani na wale wanaozalia hospitali. Akina mama vijana yaani walio na mimba za mwanzo na wale wanaoishi mijini wanatumia huduma za kuzalia hospitali zaidi kuliko wale wanaojifungua mimba za baadaye, walio na umri mkubwa na wanaoishi vijijini. Inavyoonekana ni kuwa akina mama wakishaendelea kujifungua basi hupunguza kuzalia hospitali na badala yake hujifungulia nyumbani.
Akina mama wenye elimu kwa mfano wale ambao wamesoma mpaka sekondari na vyuo vikuu wana uwezekano wa mara mbili wa kujifungulia hospitali na kujifungua huko wakisaidiwa na daktari au nesi kuliko akina mama ambao hawana elimu.
Vifo vya kina mama wakati wa mimba na kujifungua
Vifo vya kina mama vinavyohusiana na uzazi ni vifo vinavyotokea wakati wa mimba, wakati wa kujifungua au miezi miwili baada ya kujifungua.
UHAJ wa 2010 ilionyesha kuwa vifo vya kina mama wakati wa mimba au kujifungua ni kiasi cha kumi na saba kwa mia (17%) ya vifo vyote vya kina mama wa miaka (15-49).  Riski ya kupoteza maisha wakati wa mimba na kujifungua ni 0.8 kwa kila akina mama 1,000
Vifo vya kinamama wakati wa kujifungua au kwa lugha ya kitaalamu ‘Maternal Mortality Ratio’ ni vifo 454 kwa kila wanawake laki moja (100,000) wanaojifungua watoto hai. Turahisishe hii takwimu kwa kusema kuwa katika wanawake 2,000 wanaojifungua watoto hai mwanamke mmoja hufariki. Kiwango hiki cha 454/100,000 ni pungufu ya kiwango kilichoonekana kwenye UHAJ wa 2004-05 ulioonyesha takwimu ya 578/100,000 na ya 1996 iliyoonyesha 529/100,000
Kama unavyoona takwimu hii na namba ya akina mama wanaokufa wakati wa mimba na kujifungua ilionyesha kuongezeka kutoka 529/100,000 mwaka wa 1996 na kuongezeka mpaka 578/100,000 mwaka wa 2004/05 na sasa mwaka wa 2010 imepungua kufikia 454 /100,000. Kwa hiyo imepungua hata kupitiliza na kuwa chini zaidi ya mwaka  1996 ilipokuwa  529/100,000. Kupungua  kwa takwimu hii ya  idadi ya vifo vya akina mama wenye mimba na wanaojifungua ni ishara nzuri kuwa jitihada zinazofanyika kupunguza vifo vya kina mama na watoto wachanga zinaanza kufanikiwa. Pamoja na kupungua idadi hii bado iko juu sana na haivumiliki. Kifo cha mzazi, hata kikiwa kimoja hakivumiliki. Ni muhimu kuziendeleza na kuzifikisha kwa wanaozihitaji hasa kwa wale wanaoishi vijijini.

Washkaji:
Mshikaji 1: Unajua mke wangu; hii ni mimba ya tatu na anasema eti atajifungulia nyumbani. Alizalia hospitali mimba ya kwanza na hakukuwa na matatizo. Na ya pili vile vile wala hakukuwa na matatizo. Sasa anasema maana hakuna matatizo basi hii atazalia nyumbani
Mshikaji 2: Duu! Kumbe ule utafiti wa UHAJ unavyosema ni kweli kabisa kuwa wanawake wanavyoendelea kuzaa ndivyo wanavyopunguza kuzalia hospitali. Kuzalia nyumbani ni jambo la hatari kabisa maana huwezi kujua matatizo yatakapojitokeza. Wanatuambia eti matatizo wakati wa mimba yanazidi kadiri mimba zinavyozidi kuwa nyingi kwa mama mmoja. Kumbe mojawapo ya sababu za akina mama kufariki wakati wa kujifungua ni kuwa wanapoona wamezalia hospitali na hakuna matatizo, basi mimba zinazofuata wanazalia nyumbani.
Mshikaji 1: Sasa nimkubalie azalie nyumbani au azalie hospitali? Wenzake, jinsi mimba zinavyozidi kuwa nyingi ndivyo hawazalii hospitali.
Mshikaji 1: Mpeleke akazalie hospitali maana hata ikitokea huko kuwa baada ya kujifungua umerudi nyumbani bila mke na mtoto au na mtoto bila mama hutalaumiwa lakini kama hayo yakitokea hapa nyumbani! Sijui

Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK)


Tunaelezea kwenye safu hii maambukizi yanayosambazwa kwa kujamiana. Wasomaji wengi wamezoea kuyaita magonjwa ya zinaa lakini habari hii inataka tubadilishe tuyaite ‘Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK)’ na tutaelezea kwa nini.
 Wanaojua Kizungu labda watakumbuka kuwa hapo awali tulikuwa tunaita hali hizi ‘Sexually Transmitted Diseases (STD). Ukitafsiri moja kwa moja maana yake ni Magonjwa Yanayoambukizwa Kujamiana . Tuliacha kuyaita STD na sasa tunayaita ‘Sexually Transmitted Infections’ (STI) yaani Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana.
Kuna tofauti kati ya magonjwa (diseases) na maambukizi (infections) kwa kuwa magonjwa mengine yanasababishwa na maambukizi. Kwa hiyo tofauti kati ya magonjwa na maambukizi ni kuwa maambukizi yanazaa magonjwa. (Tofauti kati ya yai na kuku ni kwamba kuku anataga  yai).
‘Sexually Transmitted Infection’ (STI)  kwa Kiswahili cha moja kwa moja ni Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana. Sexually transmitted Diseases (STD)  ni Magonjwa Yanayoambukizwa kwa Kujamiana. Utaona kuwa hapa  kuna tofauti kati ya magonjwa (diseases) na maambukizi (infections) Tatizo hapa siyo la ugonjwa tu bali ni la maambukizi. Kunaweza kukawa na maambukizi yanayotokana na  kujamiana ambayo unayaona  maambukizi yenyewe, yaani unaona wadudu ambao mtu ameambukizwa kwa kujamiana, lakini huoni ugonjwa wenyewe. Hii inatokea wa mfano mtu anapoambukizwa na chawa wakati wa kujamiana  (chawa wa mafuzi). Unawaona chawa wenyewe lakini huoni ugonjwa.
Kwenye  tatizo la UKIMWI mtu anaambukizwa  na VVU. Haya ni maambukizi. Ugonjwa hauonekani moja ka moja bali kinachoonekana ni syndroma (dalili nyingi nyingi) inayosababishwa na magonjwa tegemezi yanayouvamia mwili baada ya kinga ya mwili kupungua. Maambukizi mengine kwa mfano ya kisonono na kaswende; ugonjwa unaonekana. Kwa sababu hizi za kuwa kuna hali nyingine ambapo ugonjwa hauonekani moja kwa moja na kwa kuwa katika hali zote kuna maambukizi basi ikakubalika hali hizi ziitwe Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (Sexually Transimitted Infections - STI)  Magonjwa Yanayosambazwa kwa Kujamiana (Sexually Transimitted  Diseases - STD)
Ni  Maambukizi ya Sinaa (MYS) au ni Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK)?
Ni lazima tuwashukuru wataalamu wanaojitahidi kutafsiri maneno yetu ya kisayansi kuyaweka kwenye lugha ya Kiswahili. Tushukuru kuwa tafsiri zao nyingi ni sawa na rahisi kuzitumia lakini kuna tafsiri ambazo wao wametupa kianzio ili na sisi tufikirie tuone kama zinahitaji kuboreshwa. Moja ya tafsiri ambayo inahitaji kuboreshwa ni hii ya kuziita hali hizi magonjwa. Tumeishatoa sababu hapo juu na kuelezea kuwa tuziite hali hizi maambukizi na siyo magonjwa.
Ukimwi unamtesa sana mwathirika
Kwa hiyo tuseme ni Maambukizi ya Sinaa?  Sinaa linamaanyisha starehe. Ni kama tunasema kuwa Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana yanatokana na  sinaa, yanatokana na starehe. Hapa tunakuwa kama tunasema kuwa haya ni maambukizi yanatokana na kustarehe bila hata kusema ni starehe gani - ya kunywa pombe, ya kutumia madawa ya kulevya, ya kucheza dansi na musiki - starehe zipo nyingi. Tuyaite Maambukizi Yanayosambazwa na Starehe ya Kujamiana?
Ni ukweli kuwa ukichukulia kujamiana kama starehe utapata Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana. Yanapotokea kati ya wanandoa yanatokana na mwanandoa mmoja au wote wawili kutokuwa waaminifu na kuchukulia kujamiiana kama starehe.
Ni vizuri jina la hali inayohusiana na ugonjwa unapolisikia linakueleza mengi juu ya hali yenyewe na linakuambia hata namna ya kujikinga na hali hiyo. Hapa ukisikia maneno matatu ya jina la hali hii ‘Maambukizi Yanayoambukizwa kwa  Kujamiana’ tayari umeishajua kuwa haya ni maambukizi; kuwa mwenzako anakuambukiza au wewe unamwambukiza. Ukisikia yanayosambazwa unajua kuwa yanasambazwa na siyo kwamba yanaambukizwa tu. Ukisema yanasambazwa tayari umeishasema kuwa yanaenea haraka sana kutoka mtu  hadi mtu. Ukisikia kuwa maambukizi haya yanatokana na kujamiana unaanza kujisemea ‘nijichunge sana na kujamiana ovyo ovyo.’
Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK) ni mtu kwa  mtu;  yaani yanatoka kwa mtu  mmoja yanaenda kwa mtu mwingine.  Siyo kama ilivyo kwenye ugonjwa wa kwa mfano malaria ambao vijidudu hutoka kwa mtu mmoja; vinaingia kwa mbu na baadaye kwa binadamu. Siyo kama wa kichocho ambao vijidudu vinatoka kwa mtu vinaingia kwenye konokono na baadaye vinaingia kwa mtu tena. Wataalamu wanaita hali hii ya jinsi vijidudu vinatoka kwa mwanadamu na baadaye kumrudia tena ‘mzunguko wa maambukizi’ ambapo kuna hatua mbali mbali.
Kwanza kuna wadudu wenyewe kwa mfano wanaosababisha Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana; kuna hifadhi ya hao wadudu kwa mfano hapa anayewahifadhi ni binadamu; halafu wadudu wanaingia kwa mtu mwingine na huyo mtu mwingine anawapeleka tena kwa mtu mwingine. Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana ni ya moja kwa moja kutoka kwa mtu hadi kwa mtu mwingine. Maambukizi ya magonjwa mengine yana mzunguko mrefu zaidi ambapo kuna wadudu wa maambukizi, kuna hifadhi yao ambayo moja inaweza ikawa binadamu (malaria na kichocho) au mnyama (kichaa cha mbwa); wadudu wanatoka kwenye hifadhi wanaingia kwenye mnyama mwingine kama kwa mfano kichocho kinaingia kwenye konokono, kinatoka huko na kuingia kwa binadamu. Kwa kujua mzunguko huu wa vijidudu vya magonjwa inajulikana ni wapi tuingilie ili kuuthibiti ugonjwa wenyewe. Kwa kuwa inajulikana kuwa mzunguko wa Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana ni mtu kwenda kwa mtu; na yanaambukiza kwa kujamiana, kuyakinga haya maambukizi kunahusu kuiangalia hali ya kujamiana na kuhakikisha mtu anajamiana na mwenzake ambaye hana uwezekano wa kuwa na hifadhi ya Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana (MYKK). Kuna watu ambao wana uwezekano zaidi wa kuwa hifadhi ya wadudu wa MYKK.  Kujikinga na maambukizi haya ni vema kutojamiana nao. Hawa ni watu wanaojamiana na watu wengi kwa mfano malaya au hata watu wa kawaida tu mradi wewe mwenyewe umemwangalia na kujua tabia yake. Ukishajua kuwa huyu anajamiana na wanaume au wanawake wengi au zaidi ya mmoja unajua kuna uwezekano kuwa yeye ni hifadhi ya  MYKK.
Tumeelezea ni kwa nini maambukizi haya yaitwe Mambukizi Yanayosambazwa  kwa Kujamiana na siyo Magonjwa Yanayosambazwa wa Kujamiana (STD) au Magonjwa ya Sinaa. Tuyaite Maambukizi Yanayosambazwa kwa Kujamiana au kwa kizungu STI. Wiki ujayo tutataja na kuanza kuelezea aina 13 za MYKK