Thursday 27 February 2014

Kuzaa


Vifo vya akina mama wakiwa na Mimba Vinapungua!
Utafiti wa mwaka 2010 wa Hali ya Afya ya Jamii  (UHAJ)  waonyesha mafanikio huduma za Uzazi
Utafiti wa Hali ya Afya ya Jamii 2010 (UHAJ) au kwa Kizungu DHS unaonyesha mafanikio makubwa hasa katika nyanja nne: mahudhurio  ya kliniki wakati wa kujifungua, kujifungulia hospitali, kujifungua ukisaidiwa na mhudumu wa afya yaani nesi au daktari na kupunguza vifo vya akina mama wenye mimba na wakati wa kujifungua
Kuhudhuria kliniki ya uzazi  na kupima mimba ni huduma muhimu ambapo wafanyakazi wa afya, manesi na madaktari wanampima mama na kumfuatilia ili kuyazuia matatizo yanayojitokeza wakati wa mimba, kuyatambua na kuyatibu mapema.  Kwa kupima na kufuatilia mimba kutoka inapotungwa mpaka mtoto anapozaliwa kunazuia na kupunguza matatizo yanayoweza kutokea kwa mama na mtoto wakati wa mimba, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Hapa kwetu Tanzania karibu akina mama wote wenye mimba, kiwango cha tisini na sita kwa mia (96%) hupimwa mimba yaani huhudhuria kliniki ya kina mama wenye mimba angalau mara moja wakati wakiwa na mimba. Utafiti wa Hali ya Afya  ya Jamii (UHAJ) wa   2004-05;  kiwango hiki kilikuwa tisini na nne kwa mia (94%) kwa hiyo UHAJ wa mwaka 2010  umeonyesha ongezeko kidogo  la  mbili kwa mia (2%). Ni vizuri kuona kuwa kuhudhuria kliniki wakati wa mimba ni moja ya huduma ambazo akina mama wana mwamko sana nazo wawe wa kijijini au wa mjini; wenye uwezo kiuchumi au wasio na uwezo wa kiuchumi,  wenye uwezo sana au wenye uwezo hafifu; wote huhudhuria kliniki wakati wakiwa na mimba
Mimba ya miezi saba
Usafi wakati wa kujifungua
Kujifungua kwenye hali ya usafi na pahala ambapo kuna huduma ya daktari au nesi kunapunguza sana uwezekano wa kupata matatizo wakati wa kujifungua yaani matatizo kwa mama na kwa mtoto. Inapunguza sana uwezekano wa kudhurika mama au mtoto. Mama akijifungulia nyumbani, akijifungulia mahali ambapo siyo pasafi; panapokosekana vifaa muhimu na wataalamu yaani daktari au nesi; mama na mtoto wana uwezekano wa kupata madhara ya kuumia na kupata maambukizi ya bakteria, virusi au fangasi.
Nusu ya mama wanaojifungua Tanzania yaani hamsini kwa mia (50%) huzalia kwenye kituo cha huduma za afya yaani hospitali, kituo cha afya au zahanati. Nusu yaani 50% huzalia  nyumbani. Hii tena ni ongezeko kutoka  UHAJ wa  2004-05 ulioonyesha kuwa arobaini na sita kwa mia (46%) ya akina mama wenye mimba  walikuwa wanazalia hospitali na 54% walikuwa wanazalia nyumbani.
Huyu mtoto amezaliwa sasa hivi
Kuna tofauti kati ya akina mama wanaozalia nyumbani na wale wanaozalia hospitali. Akina mama vijana yaani walio na mimba za mwanzo na wale wanaoishi mijini wanatumia huduma za kuzalia hospitali zaidi kuliko wale wanaojifungua mimba za baadaye, walio na umri mkubwa na wanaoishi vijijini. Inavyoonekana ni kuwa akina mama wakishaendelea kujifungua basi hupunguza kuzalia hospitali na badala yake hujifungulia nyumbani.
Akina mama wenye elimu kwa mfano wale ambao wamesoma mpaka sekondari na vyuo vikuu wana uwezekano wa mara mbili wa kujifungulia hospitali na kujifungua huko wakisaidiwa na daktari au nesi kuliko akina mama ambao hawana elimu.
Vifo vya kina mama wakati wa mimba na kujifungua
Vifo vya kina mama vinavyohusiana na uzazi ni vifo vinavyotokea wakati wa mimba, wakati wa kujifungua au miezi miwili baada ya kujifungua.
UHAJ wa 2010 ilionyesha kuwa vifo vya kina mama wakati wa mimba au kujifungua ni kiasi cha kumi na saba kwa mia (17%) ya vifo vyote vya kina mama wa miaka (15-49).  Riski ya kupoteza maisha wakati wa mimba na kujifungua ni 0.8 kwa kila akina mama 1,000
Vifo vya kinamama wakati wa kujifungua au kwa lugha ya kitaalamu ‘Maternal Mortality Ratio’ ni vifo 454 kwa kila wanawake laki moja (100,000) wanaojifungua watoto hai. Turahisishe hii takwimu kwa kusema kuwa katika wanawake 2,000 wanaojifungua watoto hai mwanamke mmoja hufariki. Kiwango hiki cha 454/100,000 ni pungufu ya kiwango kilichoonekana kwenye UHAJ wa 2004-05 ulioonyesha takwimu ya 578/100,000 na ya 1996 iliyoonyesha 529/100,000
Kama unavyoona takwimu hii na namba ya akina mama wanaokufa wakati wa mimba na kujifungua ilionyesha kuongezeka kutoka 529/100,000 mwaka wa 1996 na kuongezeka mpaka 578/100,000 mwaka wa 2004/05 na sasa mwaka wa 2010 imepungua kufikia 454 /100,000. Kwa hiyo imepungua hata kupitiliza na kuwa chini zaidi ya mwaka  1996 ilipokuwa  529/100,000. Kupungua  kwa takwimu hii ya  idadi ya vifo vya akina mama wenye mimba na wanaojifungua ni ishara nzuri kuwa jitihada zinazofanyika kupunguza vifo vya kina mama na watoto wachanga zinaanza kufanikiwa. Pamoja na kupungua idadi hii bado iko juu sana na haivumiliki. Kifo cha mzazi, hata kikiwa kimoja hakivumiliki. Ni muhimu kuziendeleza na kuzifikisha kwa wanaozihitaji hasa kwa wale wanaoishi vijijini.

Washkaji:
Mshikaji 1: Unajua mke wangu; hii ni mimba ya tatu na anasema eti atajifungulia nyumbani. Alizalia hospitali mimba ya kwanza na hakukuwa na matatizo. Na ya pili vile vile wala hakukuwa na matatizo. Sasa anasema maana hakuna matatizo basi hii atazalia nyumbani
Mshikaji 2: Duu! Kumbe ule utafiti wa UHAJ unavyosema ni kweli kabisa kuwa wanawake wanavyoendelea kuzaa ndivyo wanavyopunguza kuzalia hospitali. Kuzalia nyumbani ni jambo la hatari kabisa maana huwezi kujua matatizo yatakapojitokeza. Wanatuambia eti matatizo wakati wa mimba yanazidi kadiri mimba zinavyozidi kuwa nyingi kwa mama mmoja. Kumbe mojawapo ya sababu za akina mama kufariki wakati wa kujifungua ni kuwa wanapoona wamezalia hospitali na hakuna matatizo, basi mimba zinazofuata wanazalia nyumbani.
Mshikaji 1: Sasa nimkubalie azalie nyumbani au azalie hospitali? Wenzake, jinsi mimba zinavyozidi kuwa nyingi ndivyo hawazalii hospitali.
Mshikaji 1: Mpeleke akazalie hospitali maana hata ikitokea huko kuwa baada ya kujifungua umerudi nyumbani bila mke na mtoto au na mtoto bila mama hutalaumiwa lakini kama hayo yakitokea hapa nyumbani! Sijui

0 comments:

Post a Comment