Utafiti wa mwaka 2010 wa Hali ya Afya ya Jamii (UHAJ) waonyesha mafanikio huduma za Uzazi
Utafiti wa Hali ya Afya ya Jamii 2010 (UHAJ) au kwa Kizungu DHS unaonyesha mafanikio makubwa hasa katika nyanja nne: mahudhurio ya
kliniki wakati wa kujifungua, kujifungulia hospitali, kujifungua
ukisaidiwa na mhudumu wa afya yaani nesi au daktari na kupunguza vifo
vya akina mama wenye mimba na wakati wa kujifungua
Kuhudhuria kliniki ya uzazi na
kupima mimba ni huduma muhimu ambapo wafanyakazi wa afya, manesi na
madaktari wanampima mama na kumfuatilia ili kuyazuia matatizo
yanayojitokeza wakati wa mimba, kuyatambua na kuyatibu mapema. Kwa
kupima na kufuatilia mimba kutoka inapotungwa mpaka mtoto anapozaliwa
kunazuia na kupunguza matatizo yanayoweza kutokea kwa mama na mtoto
wakati wa mimba, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Hapa
kwetu Tanzania karibu akina mama wote wenye mimba, kiwango cha tisini
na sita kwa mia (96%) hupimwa mimba yaani huhudhuria kliniki ya kina
mama wenye mimba angalau mara moja wakati wakiwa na mimba. Utafiti wa
Hali ya Afya ya Jamii (UHAJ) wa 2004-05; kiwango hiki kilikuwa tisini na nne kwa mia (94%) kwa hiyo UHAJ wa mwaka 2010 umeonyesha ongezeko kidogo la mbili
kwa mia (2%). Ni vizuri kuona kuwa kuhudhuria kliniki wakati wa mimba
ni moja ya huduma ambazo akina mama wana mwamko sana nazo wawe wa
kijijini au wa mjini; wenye uwezo kiuchumi au wasio na uwezo wa
kiuchumi, wenye uwezo sana au wenye uwezo hafifu; wote huhudhuria kliniki wakati wakiwa na mimba
|
Mimba ya miezi saba
|
Usafi wakati wa kujifungua
Kujifungua
kwenye hali ya usafi na pahala ambapo kuna huduma ya daktari au nesi
kunapunguza sana uwezekano wa kupata matatizo wakati wa kujifungua yaani
matatizo kwa mama na kwa mtoto. Inapunguza sana uwezekano wa kudhurika
mama au mtoto. Mama akijifungulia nyumbani, akijifungulia mahali ambapo
siyo pasafi; panapokosekana vifaa muhimu na wataalamu yaani daktari au
nesi; mama na mtoto wana uwezekano wa kupata madhara ya kuumia na kupata
maambukizi ya bakteria, virusi au fangasi.
Nusu
ya mama wanaojifungua Tanzania yaani hamsini kwa mia (50%) huzalia
kwenye kituo cha huduma za afya yaani hospitali, kituo cha afya au
zahanati. Nusu yaani 50% huzalia nyumbani. Hii tena ni ongezeko kutoka UHAJ wa 2004-05 ulioonyesha kuwa arobaini na sita kwa mia (46%) ya akina mama wenye mimba walikuwa wanazalia hospitali na 54% walikuwa wanazalia nyumbani.
|
Huyu mtoto amezaliwa sasa hivi
|
Kuna
tofauti kati ya akina mama wanaozalia nyumbani na wale wanaozalia
hospitali. Akina mama vijana yaani walio na mimba za mwanzo na wale
wanaoishi mijini wanatumia huduma za kuzalia hospitali zaidi kuliko wale
wanaojifungua mimba za baadaye, walio na umri mkubwa na wanaoishi
vijijini. Inavyoonekana ni kuwa akina mama wakishaendelea kujifungua
basi hupunguza kuzalia hospitali na badala yake hujifungulia nyumbani.
Akina
mama wenye elimu kwa mfano wale ambao wamesoma mpaka sekondari na vyuo
vikuu wana uwezekano wa mara mbili wa kujifungulia hospitali na
kujifungua huko wakisaidiwa na daktari au nesi kuliko akina mama ambao
hawana elimu.
Vifo vya kina mama wakati wa mimba na kujifungua
Vifo
vya kina mama vinavyohusiana na uzazi ni vifo vinavyotokea wakati wa
mimba, wakati wa kujifungua au miezi miwili baada ya kujifungua.
UHAJ
wa 2010 ilionyesha kuwa vifo vya kina mama wakati wa mimba au
kujifungua ni kiasi cha kumi na saba kwa mia (17%) ya vifo vyote vya
kina mama wa miaka (15-49). Riski ya kupoteza maisha wakati wa mimba na kujifungua ni 0.8 kwa kila akina mama 1,000
Vifo vya kinamama wakati wa kujifungua au kwa lugha ya kitaalamu ‘Maternal Mortality Ratio’ ni vifo 454 kwa
kila wanawake laki moja (100,000) wanaojifungua watoto hai. Turahisishe
hii takwimu kwa kusema kuwa katika wanawake 2,000 wanaojifungua watoto
hai mwanamke mmoja hufariki. Kiwango hiki cha 454/100,000 ni pungufu ya
kiwango kilichoonekana kwenye UHAJ wa 2004-05 ulioonyesha takwimu ya 578/100,000 na ya 1996 iliyoonyesha 529/100,000
Kama
unavyoona takwimu hii na namba ya akina mama wanaokufa wakati wa mimba
na kujifungua ilionyesha kuongezeka kutoka 529/100,000 mwaka wa 1996 na
kuongezeka mpaka 578/100,000 mwaka wa 2004/05 na sasa mwaka wa 2010
imepungua kufikia 454 /100,000. Kwa hiyo imepungua hata kupitiliza na
kuwa chini zaidi ya mwaka 1996 ilipokuwa 529/100,000. Kupungua kwa takwimu hii ya idadi
ya vifo vya akina mama wenye mimba na wanaojifungua ni ishara nzuri
kuwa jitihada zinazofanyika kupunguza vifo vya kina mama na watoto
wachanga zinaanza kufanikiwa. Pamoja na kupungua idadi hii bado iko juu
sana na haivumiliki. Kifo cha mzazi, hata kikiwa kimoja hakivumiliki. Ni
muhimu kuziendeleza na kuzifikisha kwa wanaozihitaji hasa kwa wale
wanaoishi vijijini.
Washkaji:
Mshikaji 1:
Unajua mke wangu; hii ni mimba ya tatu na anasema eti atajifungulia
nyumbani. Alizalia hospitali mimba ya kwanza na hakukuwa na matatizo. Na
ya pili vile vile wala hakukuwa na matatizo. Sasa anasema maana hakuna
matatizo basi hii atazalia nyumbani
Mshikaji 2: Duu!
Kumbe ule utafiti wa UHAJ unavyosema ni kweli kabisa kuwa wanawake
wanavyoendelea kuzaa ndivyo wanavyopunguza kuzalia hospitali. Kuzalia
nyumbani ni jambo la hatari kabisa maana huwezi kujua matatizo yatakapojitokeza.
Wanatuambia eti matatizo wakati wa mimba yanazidi kadiri mimba
zinavyozidi kuwa nyingi kwa mama mmoja. Kumbe mojawapo ya sababu za
akina mama kufariki wakati wa kujifungua ni kuwa wanapoona wamezalia
hospitali na hakuna matatizo, basi mimba zinazofuata wanazalia nyumbani.
Mshikaji 1: Sasa nimkubalie azalie nyumbani au azalie hospitali? Wenzake, jinsi mimba zinavyozidi kuwa nyingi ndivyo hawazalii hospitali.
Mshikaji 1:
Mpeleke akazalie hospitali maana hata ikitokea huko kuwa baada ya
kujifungua umerudi nyumbani bila mke na mtoto au na mtoto bila mama
hutalaumiwa lakini kama hayo yakitokea hapa nyumbani! Sijui