Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz (49), ametajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa sasa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la Marekani la Forbes na
kutoa taarifa yake juzi, Rostam amekamata nafasi hiyo na ya 27 katika
Afrika akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni moja (Sh1.6
trilioni).
Mbunge huyo wa zamani wa Igunga, ameingia kwa mara ya kwanza katika
orodha ya matajiri 50 wa Afrika ya jarida hilo, pamoja na
wafanyabiashara wengine wa Tanzania, Reginald Mengi na Mbunge wa Singida
Mjini (CCM), Mohamed Dewji ‘Mo’. Katika orodha hiyo pia yumo Said
Bakhresa ambaye aliwahi kutajwa siku za nyuma.
Rostam, ambaye aliachana na siasa mwaka 2011, amempiku Bakhresa,
ambaye mwaka jana Jarida la Ventures Africa la Nigeria lilimtaja kuwa
ndiye aliyekuwa tajiri namba moja wa Tanzania. Bakhressa katika kipindi
hicho alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 620 milioni (Sh971 bilioni).
Katika orodha hiyo ya Ventures Africa, Bakhresa alifuatiwa na Rostam, Mengi na mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi anashika nafasi ya pili kwa Tanzania na ya 34 Afrika akiwa na utajiri wa Dola 550 milioni (Sh861 bilioni).
Forbes linaonyesha kuwa Bakhresa amefungana na Mo katika nafasi ya
tatu ya orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika, wote wakiwa
na utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783 bilioni).
Rostam, Mengi na Bakhresa hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo
huku Mo akisema kwamba asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa jana
alikuwa katika mapumziko ya Sikukuu ya Ashura.
Tajiri wa Nigeria, Aliko Dangote, ambaye anajenga Kiwanda cha Saruji
huko Mtwara ndiye anayeshika nafasi ya kwanza katika orodha ya Afrika,
akiwa na utajiri wa Dola20 bilioni (Sh31.7 trilioni), akifuatiwa na
familia ya Johanny Rupert ya Afrika Kusini yenye utajiri wa Dola7
bilioni (Sh10.7 trilioni) na Nick Oppenheimer, pia wa Afrika Kusini
mwenye utajiri wa Dola 6.6 bilioni (Sh10.3 trilioni).
1)Rostam Aziz
Jarida la Forbes limeripoti kuwa utajiri wa Rostam unachangiwa zaidi
na biashara ya mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi na uchimbaji wa
madini.
Anamiliki asilimia 35 ya hisa katika Kampuni ya Simu za mkononi ya
Vodacom. Ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya simu za mikononi nchini
Tanzania ikiwa na wateja zaidi ya milioni 9.5.Pia anamiliki Kampuni ya Caspian, ambayo inafanya kazi za kuchimba madini katika migodi inayomilikiwa na Kampuni za BHP Billiton na Barrick Gold.
Pia ana hisa katika Kampuni ya Hutchison Wampoa inayofanya kazi za
kupakua mizigo bandarini na anamiliki majumba nchini na katika nchi za
Mashariki ya Kati.
2) Mengi
Ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP.
Utajiri wake unatokana na kumiliki vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.
Mengi anamiliki magazeti kumi na moja, vituo vitatu vya televisheni na takriban vituo 10 vya redio.
Pia ana mgodi wa madini ya dhahabu na viwanda vya CocaCola.
Kwa mujibu jarida hilo, Mengi alizaliwa katika familia maskini na baadaye kusomea uhasibu huko Uingereza na kufanya kazi huko.
Alijiunga na Chama cha Wahasibu cha Uingereza kabla ya kurejea
Tanzania mwaka 1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Ukaguzi ya Coopers &
Lybrand Tanzania (sasa Price Water House Coopers) hadi mwaka 1989,
alipoacha kazi na kujikita zaidi katika biashara.
3) Bakhresa
Said Salim Bakhresa ni mwasisi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bakhresa Group na ana utajiri wa Dola500 milioni (Sh783 bilioni).
Ni kampuni kubwa inayoajiri zaidi ya watu 2,000 ikijishughulisha
zaidi katika kusaga nafaka, kusindika matunda, usafiri wa meli na
biashara ya mafuta. Pia kwa kutengeneza pipi na ice cream.Bakhresa aliacha shule akiwa na umri wa miaka 14 na kuanza biashara ya kuuza viazi mbatata. Baada ya hapo alifungua mgahawa na baadaye kuingia katika biashara ya kusaga nafaka.
4) Mo
Mafanikio yake yamechangiwa zaidi baada ya kuendeleza mali ya wazazi
wake. Anafanya biashara ya nyumba, kuuza mazao na viwanda vya mafuta.
Mo alirejea Tanzania baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu
cha Georgetown, Marekani na kuendeleza biashara ya maduka ambayo
yalianzishwa na baba yake.
Alinufaika baada ya kununua viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali.
Alivifanya viwanda hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua Kampuni ya
Mohamed Enterprises (MeTL) kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio
makubwa Tanzania.
Mo pia anajihusisha na biashara ya usambazaji bidhaa, viwanda vya nguo na kilimo.
Jarida hilo lilipiga hesabu za utajiri wa wafanyabiashara hao kwa
kuangalia thamani ya bidhaa zinazouzwa na kampuni zao, mikataba yao na
hasa wale walio kwenye sekta ya mafuta na ukubwa wa kampuni zao.Source:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment