Saturday, 16 November 2013

MAREKANI : TANZANIA KINARA KUNYANYASA WASICHANA, USAFIRISHAJI BINADAMU

Katika Ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu ya mwaka 2013, MAreknai imeitaja Tanzania kuwa ni kinara wa kunyanyasa wasichana, kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in Action), pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake, watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na biashara ya ngono.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka huu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu na marafiki ambao hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha au kuwatafutia ajira nzuri mijini.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka Burundi na Kenya, watu wazima kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India wanatumikishwa kufanya kazi kwenye sekta za kilimo, madini na majumbani nchini Tanzania.
Ripoti hiyo inaitupia lawama Tanzania kwa kutokuwa na sheria thabiti za kupambana na biashara haramu ya kusafirisha binadamu, huku ikitolea mfano namna ilivyoshindwa kuwasaidia raia wake waliokuwa wakinyanyaswa nje ya nchi.

0 comments:

Post a Comment