Sunday, 10 November 2013

Kimbunga Haiyan chaua zaidi ya watu 10,000 Ufilipino

Idadi ya vifo kutokana na mojawapo ya vimbunga vikali zaidi katika historia, ambacho kimeupiga mji wa katikati ya Ufilipino,Tacloban, imefikia watu 10,000. Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa nchi hiyo
Wanajeshi wakiendelea na uokozi katika eneo lililoharibiwa la uwanja wa ndege Wanajeshi wakiendelea na uokozi katika eneo lililoharibiwa la uwanja wa ndege
Mkuu wa polisi wa eneo hilo Elmer Soria amesema amepashwa taarifa na Gavana wa mkoa wa Lyete Dominic Petilla akiambiwa kuwa watu 10,000 wamekufa katika mkoa huo pekee, wengi wao wakizama majini na wengine kufunikwa na majumba yaliyoporomoka.
Takwimu za Gavana zimetokana na maafisa wa vijijini katika maeneo ambayo Kimbunga Haiyan kilipiga Ijumaa iliyopita. Kiongozi wa Mji wa Tacloban Tecson Lim amesema idadi ya vifo katika mji huo pekee huenda ikazidi 10,000.
Tacloban ni mji mkuu wa Mkoa wa Leyte wenye idadi ya watu 200,000 na mji mkubwa zaidi katika kisiwa cha Leyte. Maafisa wa Ufilipino walikuwa tayari wamewahamishia maeneo salama takribani watu 800,000 kabla ya kuwasili kimbunga hicho.
Manusura wa Kimbunga Haiyan katika mji wa katikati ya Ufilipino, Tacloban wakisubiri kuokolewa Manusura wa Kimbunga Haiyan katika mji wa katikati ya Ufilipino, Tacloban wakisubiri kuokolewa
Karibu miili 300-400 tayari imepatikana na kuna mingine mingi iliyokwama kwenye vifusi. Mazishi ya pamoja yanatarajiwa kufanyika leo katika mji wa Palo karibu na Tacloban. Kimbunga Haiyan kilifagia katika visiwa sita vya katikati ya Ufilipino siku ya Ijumaa, kwa kuyaangusha majumba wakati kikiandamana na upepo uliovuma kwa kasi ya kilometa 235 kwa saa.
Rais Benigno Aquino III amesema serikali italipa kipau mbele suala la kurejesha nishati na mawasiliano katika maeneo yaliyotengwa ili kuwezesha usambazaji wa misaada ya dharura na matibabu kwa waathiriwa.
Jamii ya Kimataifa yatuma misaada
“Marekani na serikali nyingine pamoja na mashirika yanaendesha juhudi kubwa za misaada kwa sababu ya “ukubwa wa mkasa huo”. Amesema mwenyekiti wa Shirika la Msalaba Mwekundu Richard Gordon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametuma salamu zake za rambirambi na akasema mashirika ya kiutu ya Umoja wa Mataifa yanashirikiana kwa karibu na serikali ya Ufilipino katika kushughulika na msaada wa dharura.
Kimbunga Haiyan kinatua katika pwani ya katikati ya Vitenam leo (10 Oktoba) mchana, kabla ya kupunguza kasi yake. Maafisa wa Vietnam katika mikoa minne wamewahamisha takribani watu 500,000 kutoka maeneo yenye hatari kubwa, na kuwapeleka katika majumba ya serikali, shule na makaazi mengine yenye uwezo wa kuhimili upepo mkali.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef

0 comments:

Post a Comment