Kufuatia
Rais Yoweri Kaguta Museveni kuongea kwa kumaanisha kumtaka Rais wa
Rwanda Paul Kagame kukaa meza moja na watu wanaompinga walioko DRC,
Kagame alilazimika kuitisha mkutano wa dharura na washauri wake wakuu na
kuwaeleza walichozungumza na Museveni.
Katika maongezi yake, kwa mujibu wa taarifa zilizotoka kwa mmoja wa
washauri hao Kagame alisema “nimekuwa nikiwaambia mara kwa mara kuwa
tuko peke yetu. Hata Yoweri, tuliyemwamini kama rafiki yetu na mwenzetu
anatugeuka! Leo anatuambia hiki, kesho anakwenda kukutana na viongozi
wengine na kutubadilikia.”
Baadaye akawataka washauri hao kuja na mpango mkakati wa nini cha
kufanya wakati huu Rwanda ikizidi kutengwa na nchi za Afrika na hata za
nje ya Afrika.
Kwa mujibu wa mtandao wa AfroAmerica Network, Museveni, baada ya
kurejea kutoka kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC na zile za Maziwa
Makuu (IGGLR) huko Pretoria, Afrika Kusini wiki iliyopita, alimpigia
simu Kagame na kumwambia: “Huenda sasa ni wakati muafaka wa kuzungumza
na wapinzani wako wenye silaha.”
Mwanzoni mwa mwezi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na
mwenzake wa Uingereza walimwonya Kagame kuachana mara moja na ushiriki
wake kwenye machafuko ya mashariki mwa DRC, ikiwa ni mara ya pili ndani
ya mwaka mmoja kwa wakubwa hao kutoa onyo kama hilo.
Wakati hayo yakiendelea, zipo taarifa kwamba Rais Museveni amepanga
kutuma ujumbe nchini kuja kuzungumzia mustakabali wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaambia Watanzania kwamba
Tanzania haijakiuka chochote katika makubaliano ya msingi, ila wenzetu
hao ndio huenda wana ajenda yao.
Kauli ya
Kikwete ilihitimisha hali ya wasiwasi wa Tanzania kujitoa EAC na iwapo
ujumbe wa Uganda utakuja, itakuwa ni mwendelezo wa kilichofanywa
mwishoni mwa wiki na Kenya waliomtuma Waziri wa Mambo ya Nje kuja Dar es
Salaam kuweka mambo sawa.
0 comments:
Post a Comment