HATIMA
ya Mbunge wa Urambo Magharibi Juma Kapuya (CCM), anayetuhumiwa kutishia
kumuua binti anayedaiwa kumbaka, amerejea nchini jana akitokea nchini
Sweden, huku Jeshi la Polisi likikwama kumtia mbaroni kama lilivyokuwa
likitamba.
Wakati
mbunge huyo akiwasili nchini na kupokewa na kusindikizwa na wapambe
wake, Bunge limeridhia kukamatwa kwake kwani tuhuma zinazomkabili ni za
jinai na zinamhusu yeye binafsi.
Mbunge
huyo ambaye amepata kuwa waziri, amerejea nchini jana majira ya saa
tano asubuhi kwa ndege ya Shirika la Qatar na kutua katika uwanja huo wa
ndege na kuondoka kupitia mlango wa watu maarufu (VIP).
Habari
zinasema mbunge huyo alipoondoka katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu
Julius Nyerere alikwenda moja kwa moja kwenye moja ya hoteli za jijini
Dar es Salaam na kuacha mizigo yake, kisha kuondoka na gari namba T 104
AEZ Toyota, huku wapambe wake wakiwa katika gari namba T 170 BGY aina ya
Benz.
Wakati
Kapuya akitua katika uwanja huo wa ndege, polisi ambao kwa takriban
wiki moja sasa wamekuwa wakitamba kutaka kumtia mbaroni mara baada ya
kutua, baadhi yao walionekana wakisalimiana naye kama vile hawakuwa
wanamuwinda.
Tangu
Profesa Kapuya alipoondoka nchini huku akizongwa na kashfa ya kutishia
kumuua binti anayedaiwa kumbaka, polisi wamekuwa wakitamba kutaka kumtia
mbaroni na kuahidi kuwa mara baada ya kurejea nchini mbunge huyo
angekuwa chini ya ulinzi.
Tanzania
Daima juzi liliripoti mkakati wa polisi kutaka kumtia mbaroni mbunge
huyo mara atakapotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere
jijini Dar es Salaam.
Habari
kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilisema kuwa kumekuwa na shinikizo
kutoka ndani na nje ya jeshi hilo kutaka waziri huyo wa zamani ahojiwe
kuhusiana na tuhuma zinazomkabili za kutishia kumuua binti anayedaiwa
kumbaka.
Hatua
ya polisi kutaka kumnasa Kapuya akiwa uwanja wa ndege inadaiwa
kuchangiwa na taarifa ya wiki iliyopita kwamba baadhi ya vigogo wa
jeshi hilo walishiriki kufanikisha safari ya mbunge huyo nje ya nchi
huku wakijua fika anatakiwa na polisi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alipoulizwa kuhusu ujio
wa Kapuya na kisha kuendelea kuachiwa huru, alisema yuko nje ya Jiji la
Dar es Salaam na hakuwa na taarifa za kurejea kwake.
Hata
hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Yusuph Mrefu,
alipoulizwa kuhusu sakata la Kapuya, alisema hakuwa na taarifa ya kile
kinachoendelea, kwa kuwa ndiyo kwanza amekabidhiwa ofisi.
“Mimi
niambie jambo jipya, hapa ofisini ndiyo leo nimeingia kukaimu, sasa
hayo mambo nitayajulia wapi, ni vema ungeniambia jambo jipya tuweze
kutatua,” alisema Mrefu.
Kwa
upande wake, Bunge limesema kuwa sakata la Profesa Kapuya lilifikishwa
bungeni na kubaini kuwa ni la jinai, hivyo linapaswa kwenda kwenye
mkondo wa kisheria.
Akizungumza
na Tanzania Daima jana, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila,
alithibitisha kulifahamu suala hili, kwani binti aliyedai kubakwa na
kutishiwa kuuawa na mbunge huyo alikwenda bungeni wakati Bunge la 13
lilipokuwa likiendelea mjini Dodoma.
“Suala
la binti huyo lilifikishwa ofisini kwangu kupitia kwa msaidizi wangu
ambaye alisikiliza hoja na rai yake na kushauriwa kuwa hilo ni suala la
jinai na linapaswa liende katika mkondo wa kisheria, hata hivyo binti
huyo alitambulishwa kwa Spika kama kiongozi wa wabunge na kuelekeza kuwa
tumshauri alifikishe katika mamlaka husika,” alisema Kashilila.
Tayari
binti anayedaiwa kubakwa na kutishiwa kuuawa ameshafungua jalada namba
OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam
na Jeshi la Polisi likaahidi kumkamata Kapuya popote alipo ili kujibu
tuhuma hizo zinazomkabili.
Tayari
makachero wa polisi wameanza kufuatilia namba ya simu inayodaiwa
kutumika kumtisha binti huyo na wakati mwingine kutumika kurusha pesa
kwa njia ya mtandao, zinazodaiwa kutoka kwa Profesa Kapuya kwenda kwa
binti huyo.
Credit-Tanzania Daima
Credit-Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment