Johannesburg/Dar.
Watanzania wawili wanahojiwa na Polisi wa Afrika Kusini baada ya kukamatwa jana na kilo 55 za dawa za kulevya.
Watu
hao wawili wanatazamiwa kufikishwa mahakamani kesho kujibu tuhuma za
kukamatwa na dawa hizo zenye thamani ya Rand75 milioni (Sh11.7 bilioni).
Maofisa
wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Makosa ya Jinai na Rushwa cha Afrika
Kusini (The Hawks), kiliwakamata watu hao katika Kitongoji cha Kempton
Park, Ekurhuleni, Jimbo la Gauteng.
Msemaji
wa Hawks, Paul Ramaloko alisema jana kuwa maofisa hao walivamia nyumba
waliyokuwa wanaishi Watanzania hao na kukuta mzigo huo.
Hata
hivyo, alikataa kutaja majina ya watu hao kwa kuhofia kuharibu
uchunguzi akisema bado walikuwa wanawasaka watuhumiwa zaidi wakiwamo
raia wa Afrika Kusini.
Alisema
kikosi chao kimepata mafanikio makubwa kwa kukamata dawa nyingi kiasi
hicho... “Tunakaribia kuwakamata vinara wa biashara hiyo, maana
tumeelezwa kuna kundi kubwa la watu wazito,” alisema Ramaloko. Hii
inakuwa mara ya pili katika kipindi cha miezi minne kwa Watanzania
kutuhumiwa kubeba dawa hizo.
Julai
mwaka huu, wasanii wawili Agness Gerald `Masogange’ na Melissa Edward
walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Johannesburg wakiwa
na kilo 180 za kemikali aina ya ephedrine zenye thamani ya Sh7 bilioni.
Baada
ya kukaa miezi miwili jela, Masogange alipatikana na hatia ya kuingiza
kemikali hiyo, ambayo hutumika kutengeneza dawa za kulevya na kutozwa
faini ya Rand 15,000 (Sh2.3 milioni).
Melissa aliachiwa huru baada ya kuonekana hana hatia.
Wasafirishaji sasa watumia samaki
Katika
hatua nyingine, wasafirishaji wa dawa za kulevya inasemekana wamebuni
mbinu mpya ya kutumia samaki kusafirisha bidhaa hiyo haramu.
Akizungumza
jana wakati wa uteketezaji wa dawa za kulevya, Mkuu wa Kitengo cha
Kudhibiti Dawa za Kulevya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP), Godfrey Nzowa alisema wanatumia samaki kwa kuwa wana harufu
kali.
----Mwananchi
----Mwananchi
0 comments:
Post a Comment