MWILI
wa mwanafunzi Mtanzania Jerry Mruma (23) aliyeuawa Nairobi nchini
Kenya, umewasili nchini jana na kupokelewa na ndugu, jamaa na marafiki
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Jerry
aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani (USIU)
tawi la Nairobi, aliuawa nchini humo mwishoni mwa wiki iliyopita na
anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kinondoni.
Kabla
ya maziko, ratiba ya mazishi inaonesha kuwa kutakuwa na ibada
itakayofanyika saa 7.00 mchana katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Usharika wa Mbezi Beach, lililopo eneo la Tangi Bovu.
Baadhi
ya ndugu jamaa na marafiki waliojitokeza kupokea mwili huo,
walibubujikwa machozi wakati walipokuwa wakitoa pole kwa wazazi pamoja
na wanafamilia wengine, akiwepo kaka wa marehemu Khan na mdogo wake
Kelvin.
Marehemu
ni mtoto wa aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Standard Newspapers
(TSN), wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo,
HabariLeo Jumapili na SpotiLeo Isaac Mruma.
Jerry
mbali na kuwa mwanafunzi, pia alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya
Kilimo Yetu jijini Nairobi, inayojishughulisha na masuala ya kilimo.
Kaimu
Mhariri Mtendaji wa TSN, Gabriel Nderumaki na wafanyakazi wa idara
mbalimbali waliungana uwanjani hapo kumpa pole Mruma kutokana na msiba
uliomkuta.
Wengine
waliojitokeza kuupokea mwili huo uliowasili kwa ndege ya Shirika la
Ndege la Kenya (KQ), ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
‘Mwananchi Communications’ Tiddo Muhando. Msiba huo uko nyumbani kwa
Mruma katika eneo la Mbezi Beach karibu na ghorofa za Benki Kuu.
Mwili
wa Jerry ambaye alikuwa akisoma Shahada ya Uzamili ya Utawala wa
Biashara (MBA), ulipatikana mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kijana
huyo kuripotiwa wakati akitoka katika hafla ya Usiku wa Mtanzania.
Taarifa
ya awali iliyotolewa na chuo hicho kuhusu kutoweka kwa Jerry tangu
Jumamosi iliyopita, ilisema alikuwa akitafutwa, kabla ya mwili wake
kukutwa baada ya msako ulioongozwa na Kaimu Mkuu wa Usalama wa Chuo,
Polisi na wanajumuiya wa chuo hicho.
-----Habari Leo
0 comments:
Post a Comment