UTARATIBU wa Chadema kutumia kinachoitwa
‘nguvu ya umma na vurugu’ kushinikiza sheria ipindishwe kwa maslahi
yake, umekwama kumnusuru Mbunge wa Ukerewe, Salvatory Machemli
anayetumikia adhabu ya kukaa jela kwa siku 14.
Jana Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya
Chadema, Sylvester Masinde, alikiri kuwa nguvu ya umma iliyodaiwa
kutumika kumnusuru Machemli, ni upotoshaji na hali ilivyokuwa, mamlaka
zilishajiandaa kukabiliana nao.
Kutokana na hali halisi, Masinde alisema
chama hicho hakiwezi na wala hakina mpango wa kutumia nguvu ya umma,
kushinikiza Machemli atoke mahabusu.
Masinde alifikia hatua ya kuwambia
viongozi wa ngazi ya msingi wa chama hicho kuwa ni vema utaratibu
uliowekwa kisheria uheshimiwe.
Kiongozi huyo ambaye pia ni mjumbe wa
Kamati Kuu ya chama hicho, alisema suala hilo limechunguzwa na kubaini
ni kweli Machemli aliruka dhamana, hivyo Mahakama Kuu pekee ndiyo yenye
mamlaka ya kutengua uamuzi huo.
Machemli anakabiliwa na kesi ya
uchochezi na Novemba 6 aliamriwa na Mahakama ya Wilaya kwenda rumande
kwa siku 14, baada ya kuidharau kwa kutotokea wakati kesi ikiitwa.
Tofauti na ilivyokuwa kwa Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye alisema lupango ndiko kwenye wapiga
kura wake, kwa Machemli Chadema imeamua kufuata utaratibu kumtoa.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Faustine Kishenyi aliagiza mbunge huyo
baada ya siku 14 afikishwe tena mahakamani hapo akiwa na wadhamini
wengine watatu ambao kila mmoja atatakiwa kuwa na hati ya nyumba.
Mamlaka zajiandaa Katika hatua nyingine,
kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Chadema alikiri kuwa mamlaka wilayani
humo, zilishajiandaa kukabiliana na nguvu ya umma.
Alidai alifuatana na viongozi wengine wa
chama hicho kwenda kumjulia hali mbunge huyo, lakini barabarani
walikuwa wakifuatwa kwa karibu na gari la Polisi. Hata hivyo, walipofika
gerezani, walitakiwa na Mkuu wa Gereza waondoke.
Akizungumzia sababu za kuzuiwa kuingia
gerezani hapo, kiongozi huyo alidai anahisi pengine mamlaka husika
zilitishwa na uvumi usio wa kweli kuwa zingetumika nguvu za umma
kushinikiza Mahakama itoe dhamana kwa mbunge huyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Magereza wa Wilaya,
Edward Nyabange, alisema viongozi hao wa Chadema wakiwa zaidi ya 10
walizuiwa kuingia gerezani hapo kwa sababu ya kutofuata utaratibu.
Alisema utaratibu uliopo unaelekeza
Jumapili pekee ndiyo mahabusu na wafungwa wanaruhusiwa kutembelewa na
jamaa zao na kuongeza kuwa mbali na viongozi hao kuvunja utaratibu, pia
idadi yao ilikuwa kubwa.
Source:Habarileo
0 comments:
Post a Comment