Saturday, 30 November 2013

TAZAMA UZURI WA NYUKI ULIVYO

Baadhi ya wataalamu nchini wameanza kufanya utafiti juu ya tiba hii ya nyuki katika kutibu ‘gouts’. Waswahili wanasema, mtaka cha uvunguni sharti ainame. Pia wanasema, anayependa waridi, basi avumulie miiba. Vivyohivyo, hata katika tiba, wale wanaotaka uponyaji wamejikuta wakivumilia mambo mengi yanayoleta maumivu au kukera kama vile sindano na dawa. Hivyo, usishangae kuwa kuumwa na nyuki ikawa ni tiba tosha na thabiti kwako. Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Washington, Marekani wanaeleza kuwa, sumu ya nyuki inaweza kuponya maradhi mbalimbali ikiwamo kuharibu virusi vya Ukimwi bila kuharibu seli za mwili wa binadamu. Dk Joshua Hood, kiongozi wa utafiti huo anasema, ipo sumu kali iitwayo mellitin katika mwiba wa nyuki ambayo ina uwezo wa kuingia ndani ya mfuko unaozunguka kinga ya mwili wa binadamu na kuua virusi vya Ukimwi vilivyomo ndani.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa sumu hiyo ya Mellitin iingiapo kwa wingi katika mwili wa binadamu, inaweza kuleta madhara.
Pia, Profesa Samule Wickline pia wa Marekani aliunda chembe ndogo zenye sumu ya mellitin, ambayo ina uwezo wa kuzuia saratani au dalili zozote z  vivimbe vya saratani.
Hapa nchini, Dk Augustine Godman mtaalamu wa magonjwa ya uzeeni na mshauri wa kisaikolojia anasema amejaribu kutumia tiba ya nyuki kwa wagonjwa 158 wenye matatizo kwenye viungio vya mwili (gouts), ambayo husababishwa na wingi wa tindikali ya uric katika damu.
Anasema dawa hiyo imeonyesha matokeo mazuri kwa wagonjwa wengi ambao hung’atwa na nyuki katika sehemu mbalimbali za miili yao. Dk Godman anasema, yeye humuweka mgonjwa nje ilipo mizinga ya nyuki na kisha kuwafungulia wadudu hao kutoka katika mizinga yao.
Anasema nyuki wana sumu ambayo inaingia katika mwili wa binadamu na kuondoa sumu iliyo mwilini.
Wakati huohuo, Dk Hood anasema kuwa, sumu ya nyuki ina uwezo mkubwa wa kutoa tiba na kuunda mafuta ya uke ambayo yanaweza kuzuia maambukizi ya VVU na kuviua virusi sugu.
Watafiti hao wanaeleza kuwa sumu ya nyuki ina uwezo wa kuua wale askari wakubwa wanaofanya mashambulizi katika kinga ya mwili.
nyuki
Profesa Ibadan Selako kutoka Chuo Kikuu cha Tiba Nigeria, anasema miba ya nyuki ndiyo silaha yao kuu wanayotumia wadudu hao kujilinda, kumlinda malkia na askari wengine, ni silaha ambayo ikitumiwa hata kwa binadamu inaweza kufanya maajabu.
“Mungu ameweka kitu cha ajabu katika sumu ya nyuki. Sumu hiyo inaweza kutibu mara tu nyuki anapokuuma na kuingiza miba yake katika mwili wako, baada ya dakika 45 au saa moja, nyuki hufa, na sumu aliyokuachia huingia katika mfumo wa mwili wako na kuanza kufanya maajabu,” anasema Profesa Selako.
Anasema, sumu ya nyuki inapoingia katika mwili wa mwanadamu husababisha maumivu na maumivu hayo pia huondoa maumivu. Salako anasema, ameshawahi kuwatibu watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na wengi wao wamepona kwa kutumia sumu hiyo ya nyuki.
Anasema mgonjwa huanza tiba ya kung’atwa na nyuki na huendelea na tiba hiyo kwa wiki nane hadi 12 kisha huenda kupimwa.
“Akienda kupima ataona kabisa kiwango cha virusi kwenye mwili wake kimepungua baada ya wiki nane hadi 12 za matibabu baada ya hapo tutaacha kumpa tiba, na kisha tutaendelea na tiba kwa wiki nyingine nne hadi tano, mgonjwa huenda kupima tena,” anasema
Profesa Selako anasema mgonjwa atakapokwenda kupima kwa mara ya pili, atagundua kuwa virusi katika mwili wake vinashuka kila anapoendelea na tiba na baadaye atakuta hana VVU. Anasema, nyuki wa kiume kwa kitaalamu huitwa ‘drone’ na hawana uwezo wa kutoa sumu kali kama nyuki wa kike ambao ndiyo malkia.
Shirika la Utafiti wa Ukimwi Duniani (FAIR) linasema duniani kote watu zaidi ya milioni 34 wanaishi na Virusi vya Ukimwi huku kati yao, 3.3 milioni wapo chini ya umri wa miaka 15. Wengine zaidi ya 7,000 hupata maambukizi mapya kila siku duniani.
Wakati huohuo, wanasayansi katika viwanda vya urembo duniani wamefanikiwa kutengeneza mafuta ya ngozi yenye sumu ya nyuki. Mafuta hayo ya ngozi huingia katika ngozi na kutoa sumu, kuirutubisha ngozi na kuondoa makunyanzi.
Mafuta hayo tayari yameshapata wateja  wengi, hasa baada ya Malkia Mtarajiwa, Kate Middleton kuyatumia kabla ya harusi yake na kuonyesha matokeo mazuri.
Kipodozi hicho kiitwacho Radial Bee Venom kina uwezo wa kuondoa ukavu usoni na makunyanzi na kinawasaidia zaidi watu wanaokaa katika jua kwa muda mrefu.
Dk Christopher Kim, Mkurugenzi  wa Taasisi ya Tiba ya Redbank anasema, tiba ya sumu ya nyuki iligunduliwa zaidi ya miaka 1,000 iliyopita na vielelezo vya tiba hiyo vinaonekana katika maandishi ya tiba za Ugiriki na Misri.
 Anasema tiba hiyo ilianza pindi wale wanaotunza nyuki walipoumwa mara kwa mara na wadudu hao kisha wakajisikia kupona baadhi ya maradhi kama maumivu ya kichwa, neva za fahamu, viungio vya mwili na kuwashwa.
 Kwa upande mwingine, zao la nyuki hawa yaani asali, ni tiba kwa vidonda, ngozi ya uso na huwasaidia watu wenye matatizo ya vidonda vya tumbo.
Dk Imelda Mwakitumbo wa Hospitali ya Mikocheni anasema asali ya nyuki hasa wadogo ina manufaa makubwa katika kuponya majeraha.
“Lakini pia mtu ambaye anataka kuondoa seli zilizokufa katika uso akipaka asali kwa maelekezo maalumu, anaweza kuipendezesha ngozi ya uso wake,” anasema Dk Mwakitumbo
Chanzo:Mwananch

0 comments:

Post a Comment