WAKATI anaingia madarakani rasmi Januari
20, mwaka 2009 kuiongoza Marekani, nchi kubwa yenye nguvu za kiuchumi
na kisiasa duniani, Barack Obama alikuwa na malengo mengi. Mojawapo ni
kuzidi kuipaisha Marekani na kuwasuta waliodhani nchi hiyo haiwezi
kuongozwa na mtu mweusi.
Itakumbukwa kwamba, Obama mwenye asili
ya Kenya ambaye kwa sasa ni Rais wa 44 wa Marekani, ndiye mtu wa kwanza
mwenye asili ya Afrika kuwahi kuiongoza Marekani.
Hivyo, katika kuhakikisha anatimiza
ndoto zake, alipanga safu imara ya wasaidizi, miongoni mwao aliibuka
kijana mdogo aliyekuwa na umri wa miaka 35 tu, lakini aliyekuwa na
kichwa adimu katika utundu wa kazi, hasa kwa upande wa teknolojia.
Huyu si mwingine bali ni Vivek Kundra
aliyezaliwa huko New Delhi, India. Huyu alipewa jukumu la kuwa Mkuu wa
Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Serikali ya
Marekani. Kundra, ingawa ana asili ya India, ni ‘Mswahili’ anayeijua
vyema Tanzania, kwani amekulia Tanzania.
Historia yake inaonesha kuwa, akiwa na
umri wa mwaka mmoja tu, yeye na wazazi wake, walihamia Afrika, katika
nchi ya Tanzania. Baba yake alikuwa miongoni mwa maprofesa na walimu
waliokuja nchini kufundisha katika shule kadhaa.
Kutokana na mpango huo, Kundra alijikuta
akiishi na wazazi wake huko Korogwe, Tanga na pia mkoani Dodoma. Ni
huko ndiko alikozama katika Kiswahili, akiifanya lugha yake ya kwanza
huku Kihindi na Kiingereza zikiwa lugha za ziada kwake.
Aliishi Tanzania hadi alipofikisha umri wa miaka 11 ambapo wazazi wake walihamia Washington D.C, Marekani.
“Kwa hiyo ninaijua vizuri Tanzania na
ninakifahamu vizuri Kiswahili,” anasema Kundra ambaye akiwa Marekani,
alihitimu Shahada ya Kwanza katika Saikolojia aliyoipata katika Chuo
Kikuu cha Maryland Park.
Hakuishia hapo, alirudi tena darasani
kusoma Teknolojia ya Habari katika Chuo Kikuu cha Maryland, lakini pia
alisoma katika Taasisi ya Uongozi wa Siasa ya Sorensin ya Chuo Kikuu cha
Virginia.
Kutokana na umahiri wake kitaaluma,
Machi mwaka 2011 alitangazwa kuwa mmoja wa waliothibitisha vipaji vya
uongozi duniani, akichaguliwa na jopo la wajuzi na wasomi kutoka Mkutano
wa Uchumi Duniani (WEF).
Mwaka huo, katika mkutano uliofanyika
Amman, Jordan, Kundra alikuwa mwenye furaha kukutana na kijana mwingine
aliyepewa heshima kama yake, Susan Mashibe wa Tanzania ‘milionea mtoto’
ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Kampuni ya TanJet,
kampuni ya kimataifa na ya kwanza ya aina yake nchini inayoshughulikia
masuala ya kiufundi katika ndege binafsi, za biashara na hata za
kidiplomasia.
Mwanadada huyu, pia anamiliki kampuni
nyingine inayojulikana kama Kilimanjaro Aviation Logistic Center, ambayo
inashughulikia taratibu za utuaji na urukaji wa ndege binafsi katika
Bara la Afrika.
Aidha, ameanzisha Huduma ya Matengenezo
na Ukarabati wa Ndege Kilimanjaro, kwa lengo la kutoa huduma za kisasa,
yenye kiwango na salama katika usafiri wa anga wa jumla na ushirika
katika eneo la Afrika. Lakini pia Susan ndiye Mwanamke wa Kwanza Afrika
Mashariki mwenye Cheti cha Rubani cha FAA na Mhandisi Matengenezo wa
Ndege.
Tangu kuanzishwa TanJet mwaka 2003,
Mashibe ametunukiwa Tuzo mbalimbali ikiwemo ya Askofu Desmond Tutu ya
mwaka 2009 na ile ya Mwanamke Mjasiriamali mwenye Mafanikio ya mwaka
2009.
Tukirudi kwa Kundra, mwaka mmoja kabla
ya tuzo ya WEF, alituzwa na taasisi ya teknolojia ya SANS kwa kuwezesha
kufichua wizi wa dola za Marekani milioni 300 (Sh bilioni 450) uliokuwa
unafanywa kwa njia ya mtandao kwa takribani kila mwaka na baadhi ya
watendaji serikalini.
Aidha, Kundra amewahi kutunukiwa Tuzo
kemkem kutokana na umahiri wake katika miundombinu ya teknolojia na
habari na mawasiliano, akiwa amegundua mifumo kadhaa ya kisasa. Ndiyo
maana Chuo Kikuu cha Harvard hakikutaka kuuachia ujuzi wake, na hivyo
kuamua kuingia naye mkataba wa kufundisha kwa mkataba chuoni hapo.
Nje ya kazi hiyo, Kundra pia ni Makamu
Mwenyekiti wa kampuni kubwa ya masomo ya Salesforce ya Marekani.
Majukumu mengine ya kitaaluma aliyokuwa nayo kabla ya kuitwa Ikulu ya
Marekani kumsaidia Rais Obama ni kuwa Mkurugenzi wa Miundombinu ya
Teknolojia huko Arlington, Virginia mwaka 2001 na miaka mitano baadaye,
aliteuliwa na Gavana wa Virginia, Tim Kaine kuwa mkuu wa shughuli za
kiteknolojia jimboni humo.
Ilipofika Machi 27, 2007, Meya wa Columbia, Adrian Fenty alimteua Kundra kuwa Ofisa Teknolojia Mkuu wa Columbia.
Je, anazungumziaje kuaminiwa kwake na
Rais Obama? Anasema: “Ni heshima kubwa. Sikuwaza kuwa msaidizi wa Rais
katika nchi muhimu kama Marekani. Kama unavyojua, nilizaliwa India,
nikakulia Tanzania.
Ni mhamiaji tu hapa na ikumbukwe nilikuja Marekani mwaka 1985 nikiwa sijui hata Kiingereza, zaidi ya Kihindi na Kiswahili.
“Lakini bidii katika masomo na nyanja ya
utawala, vitu nilivyorithi kutoka kwa wazazi wangu, ndivyo
vilivyonifikisha hapa, kiasi cha kuaminika na jamii na hata Rais wa
nchi.Namshukuru Mungu kwa kila jema linalotendeka juu yangu. Namshukuru
Rais Obama kwa kuwapa nafasi vijana pia.”
Huyo ndiye Vivek Kundra, mtaalamu wa
teknolojia ya habari na mawasiliano aliyekulia Tanzania, lakini sasa
akifanya vitu vikubwa nchini Marekani.
Source: HabariLeo
0 comments:
Post a Comment