HUKUMU
ya kesi ya matumizi mabaya ya ofisi katika utoaji wa kibali cha ujenzi
wa jengo la ghorofa 18 karibu na Ikulu Dar es Salaam, inayowakabili
vigogo wawili wa Wakala wa Ujenzi itatolewa Januari 15 mwakani.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Sundi Fimbo alisema hayo jana baada ya washitakiwa kumaliza kujitetea.
Washitakiwa
katika kesi hiyo ambao wamejitetea bila kuita mashahidi ni Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na Msanifu
Mkuu wake Richard Maliyaga.
Ikulu inavyoonekana ukiwa juu ya jengo.
Awali
akijitetea Maliyaga alidai kuwa, Mkurugenzi wa Miliki wa Wakala,
Charles Makungu ndiye aliyekuwa na uamuzi wa mwisho wa kutoa kibali cha
ujenzi na kupeleka barua katika halmashauri husika na kwa waleta maombi.
Akiongozwa
na Wakili Majura Magafu, Maliyaga alidai alikuwa Mwenyekiti wa Kamati
ya Kutoa Vibali na walipopata ombi la ujenzi huo walipitia michoro na
baada ya kuona ipo sawa alisaini kibali na kupeleka kwa Makungu.
Alidai
kuwa awali aliandika barua akipendekeza ofisi ya Makungu iombe kibali
kutoka Halmashauri ya Ilala lakini hakupata majibu hadi alipopewa
maelekezo kutoka katika kamati inayoshughulikia miradi ubia kuwa watoe
kibali hicho. Alidai alikataa kutoa kibali hicho lakini baada ya
wanakamati kujadili walikubali kufuata maelekezo hayo na kutoa kibali
hicho.
"Sisi
hatukuhusika katika kutoa uamuzi wa mradi huu, mimi nimeonewa kwasababu
sijanufaika na sikutumia madaraka yangu vibaya na nashangaa kwanini
Makungu, watu kutoka katika kamati yetu au ile ya miradi ya ubia
hawajaletwa mahakamani," alidai Maliyaga.
Katika
utetezi wake hivi karibuni Kimweri alidai kuwa amefunguliwa kesi hiyo
kwa kuwa alikuwa na ugomvi na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli baada ya
kumchafua kwenye vyombo vya habari.
Alidai
ugomvi huo ulitokana na mchakato wa uuzwaji wa nyumba za Serikali
ambapo yeye alikataa kusaini mkataba wa kumuuzia nyumba mwanafunzi kwa
sababu hakustahili ndipo Magufuli alipodhani kuwa alitoa taarifa hizo
kwenye vyombo vya habari.
Kimweri
na Maliyaga wanakabiliwa na mashitaka matano ya matumizi mabaya ya
ofisi katika utoaji kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 15 kiwanja
namba 45 mtaa wa Chimara.
Aidha wanadaiwa kutoa kibali kingine cha kuongeza ujenzi kutoka ghorofa 15 hadi 18.
-habarileo
0 comments:
Post a Comment